Ana səhifə

Taarifa ya tume ya taifa ya uchaguzi kuhusu uchaguzi wa rais, wabunge na


Yüklə 4.81 Mb.
səhifə20/33
tarix26.06.2016
ölçüsü4.81 Mb.
1   ...   16   17   18   19   20   21   22   23   ...   33

Kuhesabu Kura


Kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi na Maelekezo ya Tume, Wasimamizi wa Vituo ndio wahusika wakuu wa zoezi la Kuhesabu Kura katika Vituo vya Kupigia Kura. Mawakala, Msimamizi wa Uchaguzi, Watazamaji wa Uchaguzi, Mjumbe wa Tume na wengine waliotajwa katika Sheria wanaruhusiwa kuwepo kushuhudia zoezi la kuhesabu Kura.
Utaratibu wa kuhesabu Kura kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi hufanyika hapo hapo Kituoni mara baada ya kukamilika kwa zoezi la upigaji Kura na kufunga Kituo.
Katika baadhi ya Vituo vya kuhesabia Kura kulijitokeza matukio ya kuvamiwa na washabiki wa Vyama vya Siasa kutokana na madai kuwa Watendaji walikuwa wanachelewa kutangaza matokeo. Matukio hayo yalisababisha kujeruhiwa kwa baadhi ya Watendaji, uharibifu wa vifaa vya Uchaguzi na mali nyingine.
      1. Fomu za Matokeo na Ujazaji wake


Baada ya kukamilisha zoezi la kuhesabu Kura, Fomu za Matokeo zilijazwa na Msimamizi wa Kituo na kusainiwa na Mawakala wa Vyama vya Siasa au Wagombea. Fomu za Matokeo zilizojazwa na kusainiwa na Wasimamizi wa Vituo, na kusainiwa na Mawakala wa Vyama vya Siasa au Wagombea ni Fomu Na. 21A, Fomu Na. 21B na Fomu Na. 21C. Vile vile katika zoezi la kuhesabu Kura zipo Fomu zingine ambazo zilijazwa na Wasimamizi wa Vituo na Mawakala. Fomu hizo ni Fomu Na. 16 na 20. Fomu za Matokeo zilikuwa katika vijitabu badala ya kuwa moja moja kama ilivyokuwa katika Chaguzi zilizopita. Katika Fomu za Matokeo ya Uchaguzi kituoni kwa Uchaguzi wa mwaka 2010 zilikuwa zimegawanyika katika sehemu mbili yaani sehemu ‘A’ na sehemu ‘B’.
Kwa upande wa sehemu ‘A’ Fomu hizo zilijazwa matokeo ya Uchaguzi kama yalivyojitokeza vituoni. Sehemu ‘B’ ilijazwa tu endapo kulikuwepo na Kura zenye mgogoro ambapo hatimaye zilikwenda kukamilishwa katika hatua ya ujumlishaji wa Kura.
Baada ya kuhesabu Kura na kujaza Fomu za Matokeo, nakala za Fomu hizo zilibandikwa nje ya Kituo na Mawakala kupatiwa nakala, na nyingine kupelekwa kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimboni na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kwenye Kata kwa ajili ya zoezi la Kujumlisha. Fomu za Matokeo ziliwekewa alama za usalama ili kudhibiti uwezekano wa kughushiwa.
Mara baada ya kukamilika kwa Uhesabuji wa Kura na Utangazaji wa Matokeo katika Kituo cha Kupigia Kura, masanduku ya Kura, vifaa mbalimbali vya Uchaguzi na Matokeo ya Uchaguzi yalipelekwa katika Kituo cha Kujumlishia Kura. Msimamizi wa Kituo cha Kupigia Kura, Mawakala wa Upigaji Kura na Askari ndio waliopeleka vifaa hivyo katika Kituo cha Kujumlishia Kura.
      1. Utoaji wa Taarifa ya Matokeo Katika Vituo


Wasimamizi wa Vituo vya Kupigia Kura, baada ya kukamilisha zoezi la kuhesabu Kura na kujaza Fomu za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais, Bunge na Madiwani, walibandika nakala moja mahali pa wazi kituoni. Aidha, walimpatia kila Wakala wa Chama/Mgombea nakala moja moja ya Matokeo ya Uchaguzi na waliwapatia Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wa Kata nakala moja ya Matokeo ya Uchaguzi wa Madiwani. Pia waliwapatia Wasimamizi wa Uchaguzi nakala za Matokeo ya Uchaguzi wa Rais na Uchaguzi wa Bunge kwa ajili ya kutumika wakati wa kujumlisha Kura.
Kwa ujumla zoezi la Kuhesabu Kura katika Vituo lilifanyika kwa uwazi na hivyo kumalizika kwa amani. Wakala wa Vyama Vya Siasa/ Wagombea waliokuwepo Vituoni walipata nakala za matokeo. Mawakala wengi walisaini Fomu za Matokeo.
Baada ya zoezi hilo kukamilika lilifuatiwa na Usafirishaji wa Masanduku ya Kura, Vifaa vya Uchaguzi na Matokeo ya Uchaguzi ya Kituo kwenda mahali ambapo ujumlishaji wa Kura ulipangwa kufanyika. Kwa hiyo, matokeo ya Uchaguzi wa Madiwani yalipelekwa Ofisi ya Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata kwa ajili ya kujumlisha Kura za Uchaguzi wa Diwani wa Kata husika. Aidha, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi mmoja kutoka kila Kata alipeleka matokeo ya Uchaguzi wa Wabunge na Uchaguzi wa Rais kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo kwa ajili ya Kujumlishwa.
    1. Changamoto Zilizojitokeza


  1. Viwango vidogo vya malipo ya posho za Watendaji wa Uchaguzi ukilinganisha na uzito na unyeti wa kazi zao.

  2. Muda mfupi wa Mafunzo kwa Watendaji kutokana na ufinyu wa Bajeti.

  3. Baadhi ya Vituo kuwa mbali sana na Wapiga Kura.

  4. Mwitikio mdogo wa Wapiga Kura kwenda Vituoni kuangalia orodha za Wapiga Kura zilizobandikwa ili kutambua Vituo walivyopangiwa kupigia Kura Siku ya Uchaguzi.

  5. Wapiga Kura wachache kujitokeza Kupiga Kura ikilinganishwa na waliojiandikisha.

  6. Baadhi ya Wapiga Kura Majina yao kutokuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

  7. Baadhi ya Mawakala hawakusaini matokeo baada ya kuona Vyama vyao/ Wagombea wao hawajafanya vizuri. Hata hivyo zoezi la kukamilisha taratibu nyingine liliendelea.

  8. Baadhi ya Wasimamizi wa Vituo hawakuelewa vizuri maelekezo ya ujazaji wa Fomu za Matokeo, kwa mfano wengine hawakujaza Matokeo ya Wagombea ambao hawakupata hata Kura moja na wengine walijaza matokeo katika sehemu ‘B’ ya Fomu ya Matokeo badala ya Sehemu ‘A’.

  9. Baadhi ya Mawakala kutozingatia Maelekezo ya Tume ya kutonakili majina na namba za Wapiga Kura kituoni jambo ambalo lilileta hofu kwa baadhi ya Wapiga Kura na kupunguza kasi ya uendeshaji Uchaguzi kituoni.

  10. Baadhi ya nakala za Fomu za Matokeo zilikuwa hazionyeshi tarakimu vizuri kutokana na kuwa baadhi ya Wasimamizi wa Vituo kutogandamiza kalamu vya kutosha jambo ambalo lilileta usumbufu kwa baadhi ya Mawakala.

  11. Mafunzo ya Mawakala kutolewa na watu wa nje ya nchi wasio na uelewa wa kutosha kuhusiana na Sheria za Uchaguzi na mazingira ya Tanzania.


SURA YA SITA

KUJUMLISHA KURA NA KUTANGAZA MATOKEO YA UCHAGUZI




    1. Utaratibu wa Kujumlisha Kura Katika Majimbo na Kata


Utaratibu wa Kujumlisha Kura ulifanyika baada ya masanduku ya Kura na matokeo ya Uchaguzi, kutoka katika Vituo vya Kupigia Kura kupokelewa katika Kituo cha Kujumlishia Kura.
Ujumlishaji wa Kura za Rais na Wabunge ulifanyika katika Makao Makuu ya Halmashauri, kwa kutumia Mfumo wa Kujumlishia Matokeo ambapo Matokeo ya Uchaguzi, katika Fomu Na. 21A na 21B yaliingizwa katika Kompyuta baada ya kufanyiwa Scanning. Vile vile, Mfumo huu ndio ulitumika kuyatuma matokeo moja kwa moja katika Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi mjini Dar es Salaam kupitia njia ya mtandao wa kompyuta.
Ujumlishaji Kura za Udiwani ulifanyika katika Kata ambapo ulisimamiwa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Kata. Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Kata baada ya kupokea masanduku ya Kura na matokeo toka vituoni alijumlisha Kura za Udiwani katika Kata. Baadaye alipeleka taarifa za matokeo hayo pamoja na masanduku na Matokeo ya Uchaguzi toka vituoni na vifaa vingine vilivyohusika na Uchaguzi wa Rais na Bunge kwa Msimamizi wa Uchaguzi ili ujumlishaji ufanyike.
Katika ujumlishaji huo Msimamizi wa Uchaguzi alielekezwa na Tume kuanza na Matokeo ya Uchaguzi wa Rais, na kufuatiwa na ujumlishaji wa matokeo ya Uchaguzi wa Mbunge/ Wabunge. Mara baada ya kukamilisha ujumlishaji wa matokeo ya Rais alijaza Fomu ya Matokeo ya Uchaguzi wa Rais (Fomu Na. 24A) na alituma matokeo hayo Tume kwa kutumia Mfumo wa kompyuta wa Menejimenti ya matokeo ya Uchaguzi.
Zoezi la kujumlisha Kura za Uchaguzi wa Rais na Wabunge lilifanywa na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya kuhakikisha kuwa:-

  1. Amepokea masanduku yote ya Kura za Rais na Wabunge kwa Vituo vyote vya Kupigia Kura na Matokeo yake ya Uchaguzi.

  2. Mawakala au Wagombea wamewasili katika kituo cha kujumlishia Kura na wamepewa fursa ya kutoa maelezo kuhusu matukio muhimu yaliyojitokeza katika zoezi la Uchaguzi ambayo Msimamizi wa Uchaguzi hajayaeleza. Hata hivyo, pale ambapo Mawakala au Wagombea hawakuwepo ujumlishaji uliendelea kwa kuzingatia Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

  3. Ameshughulikia kutatua Kura zenye mgogoro ambapo kwa madhumuni ya Uchaguzi wa mwaka 2010, Fomu Na. 21A Sehemu B kwa Uchaguzi wa Rais na Fomu Na. 21B Sehemu B kwa Uchaguzi wa Wabunge zilijazwa na kusainiwa na Mawakala zikionesha hali halisi ya Matokeo baada ya kushughulikia Kura zenye mgogoro.

Katika Majimbo yote ya Uchaguzi 239, Mfumo wa Kompyuta wa Menejimenti ya Matokeo ya Uchaguzi ulifanya kazi na ulitumika kwa mafanikio katika Majimbo 150 katika kujumlisha Kura, lakini kati ya hayo ni Majimbo 113 yaliutumia kutuma Matokeo ya Uchaguzi Makao Makuu ya Tume. Majimbo mengine 37 yalituma Matokeo kwa kutumia nukushi (fax). Aidha, Majimbo mengine 89 hayakuweza kabisa kutumia Mfumo huo wa Ujumlishaji na badala yake yalitumia Mifumo mingine kama Exel Spreadsheet.


1   ...   16   17   18   19   20   21   22   23   ...   33


Verilənlər bazası müəlliflik hüququ ilə müdafiə olunur ©atelim.com 2016
rəhbərliyinə müraciət