Ana səhifə

Taarifa ya tume ya taifa ya uchaguzi kuhusu uchaguzi wa rais, wabunge na


Yüklə 4.81 Mb.
səhifə4/33
tarix26.06.2016
ölçüsü4.81 Mb.
1   2   3   4   5   6   7   8   9   ...   33

SURA YA KWANZA




UTANGULIZI

    1. Tanzania


Tanzania ni Muungano wa sehemu mbili ambazo ni Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Tanzania imegawanywa katika mikoa 26 kati ya hiyo mikoa 21 ipo Tanzania Bara na mikoa 5 ipo Tanzania Zanzibar. Nchi ina Majimbo ya Uchaguzi 239 ambapo 189 yapo Tanzania Bara na 50 yapo Tanzania Zanzibar.
    1. Mfumo wa Siasa wa Tanzania


Kwa mujibu wa Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, nchi ya Tanzania ni nchi ya Kidemokrasia yenye kufuata Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa kuanzia Julai, 1992.

Kwa sasa kuna Vyama vya Siasa kumi na nane (18) vilivyopata usajili kamili ambavyo ni: African Farmers Party (AFP), African Progressive Party of Tanzania (APPT – Maendeleo), Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Haki na Ustawi Tanzania (CHAUSTA), Civic United Front (CUF), Democratic Party (DP), JAHAZI ASILIA, Demokrasia Makini (MAKINI), National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi), National League for Democracy (NLD), National Reconstruction Alliance (NRA), Sauti ya Umma (SAU), Tanzania Democratic Alliance (TADEA), Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP), Union for Multi-Party Democracy (UMD) na United Peoples Democratic Party (UPDP).


    1. Mfumo wa Uchaguzi Katika Tanzania


Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unatumia mfumo wa mgombea anayepata kura nyingi kuliko wagombea wengine kutangazwa mshindi (First-Past-the-Post). Aidha, kuna Wabunge wa Viti Maalum vya Wanawake wanaopatikana kwa kutumia mfumo wa uwiano wa Kura (Proportional Representation) ambazo kila Chama kimepata katika Uchaguzi wa Bunge nchi nzima. Madiwani wa Viti Maalum vya Wanawake wanapatikana kwa kutumia mfumo wa uwiano wa Viti vya Udiwani ambavyo kila Chama kimeshinda katika Halmashauri husika.

Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, Tanzania ilifanya Uchaguzi Mkuu wa nne tarehe 31 Oktoba, 2010. Uchaguzi huo ulijumuisha Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Madiwani wa Tanzania Bara zilizofanyika kwa pamoja chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Aidha, Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Baraza la Wawakilishi, na Madiwani wa Zanzibar ulifanyika tarehe hiyo hiyo chini ya usimamizi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.


Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji hufanyika Tanzania Bara chini ya usimamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) kabla ya Uchaguzi Mkuu. Kwa upande wa Zanzibar Masheha huteuliwa na Wakuu wa Mikoa.
    1. Mzunguko wa Uchaguzi (Election Cycle)


Uchaguzi unajumuisha shughuli mbalimbali zinazofanyika wakati wote katika mzunguko wa miaka mitano (Election Cycle). Mara baada ya kukamilisha Uchaguzi Mkuu Tume inaendelea na kazi mbalimbali zikiwemo kuandaa na kutoa Taarifa ya Uchaguzi, kufanya tathmini ya Uchaguzi uliopita, kuhusika kwa pamoja na Serikali katika kujibu malalamiko ya kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Bunge na Madiwani, kupitia na kuandaa Mpango Mkakati unaojumuisha uendeshaji wa Chaguzi zitakazofuata, kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha na vifaa, kufanya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kutoa Elimu ya Mpiga Kura, kufanya mapitio ya Sheria za Uchaguzi, Kanuni na Maelekezo ya Tume ili kuyaboresha, na kupata uzoefu wa usimamiaji Uchaguzi kutoka nchi mbalimbali zinazofanya Uchaguzi kama inavyoonekana katika Mchoro Na. 1

Mchoro Na. 1: Mzunguko wa Shughuli za Uchaguzi

Chanzo: Kitabu cha Electoral Management Design: The International IDEA Handbook, 2006 uk.16.
    1. Tume ya Taifa ya Uchaguzi


Mchakato wa Uchaguzi katika mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, sharti uendeshwe na kusimamiwa na chombo kinachojitegemea, kilichopewa mamlaka kamili. Kwa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani wa Tanzania Bara.
      1. Muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi


Tume ina Wajumbe saba ambao huteuliwa na Rais kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Wajumbe hao saba ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe watano. Vile vile ina Katibu wa Tume/Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia huteuliwa na Rais. Katibu wa Tume ndiye Mtendaji Mkuu wa Tume.
Tume kwa sasa inaongozwa na Mhe. (Mst.) Jaji Lewis M. Makame ambaye ni Mwenyekiti na Mhe. Jaji Omar O. Makungu 1ni Makamu Mwenyekiti wa Tume. Wajumbe wengine ni Mhe. Prof. Amon E. Chaligha, Mhe. Hilary J. Mkatte, Mhe. Mchanga H. Mjaka, Mhe. (Mst.) Jaji John J. Mkwawa na Mhe. (Mst.) Jaji Mary H.C.S Longway. Aidha, Bw. Rajabu R. Kiravu ni Katibu wa Tume na Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Sifa za kuwa Mjumbe wa Tume kwa mujibu wa Ibara ya 74(1) ni zifuatazo: Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume wanatakiwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufaa au ni watu wenye sifa ya kuwa Wakili na wamekuwa na sifa hizo kwa muda usiopungua miaka kumi na tano. Kulingana na Katiba, Mwenyekiti akitokea sehemu moja ya nchi, Makamu atatokea sehemu ya pili ya nchi. Aidha, kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kimeeleza sifa za Wajumbe wengine kwamba mmoja atatoka Chama cha Mawakili wa Tanganyika (Tanganyika Law Society) na wengine wanne watateuliwa kwa kuzingatia kuwa na uzoefu wa kutosha katika uendeshaji au usimamizi wa Uchaguzi kama Rais atakavyoona inafaa.
Aidha, Tume ni Chombo kinachojitegemea na ina Watumishi ambao wanaongozwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi. Tume kwa sasa ina Watumishi 119 Makao Makuu ya Tume na haina Watumishi wa Kudumu katika Mikoa na Halmashauri nchini.

      1. Majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi


Majukumu ya Tume ni:-

  1. Kusimamia na kuratibu Uandikishaji wa Wapiga Kura katika Uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

    1. Kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Rais na Wabunge;

    2. Kuchunguza Mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya Uchaguzi wa Bunge;

    3. Kusimamia na Kuratibu Uandikishaji Wapiga Kura na uendeshaji wa Uchaguzi wa Madiwani katika Tanzania Bara;

    4. Kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima, Kuratibu na Kusimamia Taasisi na watu wanaotoa Elimu hiyo;

    5. Kuteua na kuwatangaza Wabunge na Madiwani wa Viti Maalum vya Wanawake; na

    6. Kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge.
1   2   3   4   5   6   7   8   9   ...   33


Verilənlər bazası müəlliflik hüququ ilə müdafiə olunur ©atelim.com 2016
rəhbərliyinə müraciət