Ana səhifə

Taarifa ya tume ya taifa ya uchaguzi kuhusu uchaguzi wa rais, wabunge na


Yüklə 4.81 Mb.
səhifə3/33
tarix26.06.2016
ölçüsü4.81 Mb.
1   2   3   4   5   6   7   8   9   ...   33

DIBAJI

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika tarehe 31 Oktoba, 2010 ambao ulikuwa ni Uchaguzi Mkuu wa nne chini ya Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa.


Taarifa hii inakusudia kueleza namna Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ulivyoendeshwa, mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na mapendekezo mbalimbali ya kuboresha uendeshaji wa Uchaguzi ujao.
Taarifa hii ina Sura tisa (9) zifuatazo:-


  1. Utangulizi

  2. Maandalizi ya Uchaguzi

  3. Uandikishaji na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

  4. Uteuzi wa Wagombea na Kampeni za Uchaguzi

  5. Upigaji Kura na Uhesabuji wa Kura Vituoni

  6. Kujumlisha Kura na Kutangaza Matokeo ya Uchaguzi

  7. Ushiriki wa Wadau wa Uchaguzi

  8. Watazamaji wa Uchaguzi

  9. Hitimisho na Mapendekezo

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kutoa shukrani kwa Wadau wote wa Uchaguzi na Watendaji wote wa Uchaguzi walioshiriki katika kufanikisha Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika tarehe 31 Oktoba, 2010. Kwa upande wa Wadau wa Uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ingependa kwa njia ya kipekee kuwashukuru kwa kuwataja wafuatao:-




  1. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

  2. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

  3. Vyama vya Siasa na Wagombea wote

  4. Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)

  5. Washirika wa Maendeleo

  6. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar

  7. Jeshi la Polisi la Tanzania

  8. Tume Huru ya Uchaguzi ya Afrika Kusini

  9. Vyombo vya Habari

  10. Watazamaji wa Uchaguzi

  11. Ofisi ya Taifa ya Takwimu

  12. Asasi mbalimbali za Kiraia

  13. Wapiga Kura wote na Wananchi kwa ujumla

  14. Jeshi la Wananchi wa Tanzania

  15. Viongozi wa Dini na Mashirika ya Kidini

  16. Msajili wa Vyama vya Siasa

  17. Watendaji wa Tume katika Ngazi mbalimbali

Ni matarajio ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Taarifa hii itakidhi matarajio ya wasomaji mbalimbali wa ndani na wa nje ya nchi. Vile vile kwa upande wa Wadau wa Uchaguzi, watafiti wa masuala ya Uchaguzi na wasomaji wengine watanufaika sana kutokana na Taarifa hii.


MUHTASARI WA TAARIFA





    1. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ilisimamia na kuendesha Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Huu ulikuwa ni Uchaguzi Mkuu wa nne kufanyika tangu kuanzishwa tena kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa hapo mwaka 1992.




    1. Baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, hadi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Tume iliendesha na kusimamia Chaguzi ndogo za Bunge katika Majimbo sita (6) na Chaguzi ndogo za Madiwani katika Kata sabini na nne (74).




    1. Tume ya Taifa ya Uchaguzi, baada ya kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, ilifanya Uboreshaji wa Daftari hilo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Uboreshaji huo ulihusisha kuandikisha Wapiga Kura wapya waliotimiza sifa za kuandikishwa, kuwafuta Wapiga Kura wasio na sifa, kuwapatia Kadi Mpya Wapiga Kura waliopoteza au kuharibika kadi zao, kubadilisha taarifa za Wapiga Kura kutokana na sababu mbalimbali na kuhamisha Wapiga Kura waliohama kutoka Kata au Jimbo moja kwenda Kata au Jimbo jingine.

Uboreshaji huo ulifanyika katika Awamu mbili, ambapo Uboreshaji wa Awamu ya Kwanza ulifanyika kati ya tarehe 14 Januari, 2008 hadi tarehe 28 Desemba, 2008 na Uboreshaji wa Awamu ya Pili ulifanyika kati ya tarehe 31 Agosti, 2009 hadi tarehe 19 Juni, 2010.


Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulifanyika Kikanda na ulifanyika kwa siku sita kwa kila Kanda husika. Uboreshaji huo ulifanyika kwa mafanikio ambayo katika Awamu ya Kwanza ulifikia asilimia 77.3% na katika Awamu ya Pili ulifikia asilimia 96.3% ya makadirio.


    1. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya uchunguzi wa mipaka ya Majimbo ya Uchaguzi katika Majimbo mbalimbali kwa mujibu wa Matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Tume ilizingatia vigezo vilivyotajwa katika Katiba ambavyo ni idadi ya watu, upatikanaji wa mawasiliano na hali ya kijiografia. Aidha, Tume iliongeza vigezo vingine kumi (10) ambavyo kwa pamoja vilitumika katika kugawa Majimbo ya Uchaguzi. Majimbo yaliyofanyiwa uchunguzi wa mipaka na kukidhi vigezo husika ni Nkasi, Tunduru, Maswa, Kasulu Mashariki, Bukombe, Singida Kusini na Ukonga. Jumla ya Majimbo mapya saba (7) yaliongezwa na hivyo kufanya jumla ya Majimbo ya Uchaguzi katika nchi nzima kuwa 239 kutoka 232 yaliyokuwepo mwaka 2005.




    1. Ili kuwezesha Uchaguzi kufanyika kwa ufanisi zaidi, kulifanyika marekebisho mbalimbali katika maeneo ya mchakato wa Uchaguzi kuanzia Uandikishaji Wapiga Kura hadi kutangaza Matokeo. Jumla ya marekebisho 15 yalifanyika katika Sheria za Uchaguzi. Aidha, pamoja na mambo mengine kuanzishwa kwa Sheria ya Gharama ya Uchaguzi ya mwaka 2010 kulichangia kufanyika kwa marekebisho kadhaa katika Sheria za Uchaguzi.




    1. Kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume yaliyotolewa katika Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 juu ya Maadili ya Uchaguzi kupewa nguvu ya kisheria, kwa kufanya marekebisho katika Sheria ya Uchaguzi, mapendekezo hayo yalitekelezwa na Maadili hayo kupewa nguvu ya kisheria na kutumika katika Uchaguzi wa mwaka 2010.




    1. Gharama ya Uchaguzi, ikijumuisha Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na uendeshaji wa Uchaguzi ilikuwa Sh.154,560,251,132/=. Serikali ilitoa Sh. 135,635,803,145/= na Washirika wa Maendeleo walichangia Sh. 18,924,447,987/= zilizotumiwa moja kwa moja na Tume. Kwa ujumla fedha zilitolewa kwa wakati na hivyo kuwezesha shughuli kutekelezwa kulingana na Ratiba ilivyopangwa.




    1. Tume ilinunua vifaa vya Uchaguzi kwa kuzingatia mahitaji na kutumia utaratibu ulioelekezwa katika Sheria ya Manunuzi ya Vifaa vya Umma Na. 21 ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005. Vifaa vilinunuliwa kwa njia ya Zabuni ya Wazi na kwa kutumia utaratibu wa moja kwa moja. Aidha, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) lilisaidia kununua baadhi ya vifaa vilivyohusika na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na vile vilivyohusika na hatua nyingine za mchakato wa Uchaguzi.




    1. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina Makamishna saba (7) na Watendaji mbalimbali 119. Kwa madhumuni ya Uchaguzi wa mwaka 2010, Tume pia ilitumia Watumishi wa Muda 674 Makao Makuu. Katika ngazi ya Mikoa na Majimbo, Tume ilikuwa na Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa 23, Wasimamizi wa Uchaguzi 142, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo 995, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wa Kata 6,670 na Watendaji wa Vituo 212,156. Walinzi wa Vituo walikuwa 53,039.




    1. Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliwashirikisha wadau mbalimbali kwa njia ya kufanya mikutano katika hatua tofauti za Uchaguzi. Wadau hao ni pamoja na Vyama vya Siasa, Serikali, Washirika wa Maendeleo, Vyombo vya Habari, Watu wanaoishi na Ulemavu, Asasi za Kiraia na Viongozi wa Dini.

Kwa Vyama vya Siasa, Tume ilifanya mikutano tarehe 21 Aprili, 2009, 22 Januari, 2010 na 11 Oktoba, 2010 na Viongozi wa Kitaifa wa Vyama vya Siasa na mikutano na Viongozi wa Vyama vya Siasa ngazi ya Mikoa ilifanywa tarehe 18- 22/10/2010. Kwa ujumla Tume ilinufaika sana na ushiriki wa Wadau hao katika uendeshaji wa Uchaguzi na hasa kupata maoni yao, na hivyo kukuza Demokrasia.




    1. Tume iliendesha Elimu ya Mpiga Kura kwa kuzingatia Mpango Mkakati wake kwa njia mbalimbali ikiwemo kuchapisha na kusambaza mabango, vijitabu mbalimbali, ‘banners’, ujumbe katika Nyumba za Ibada, Vyombo vya Habari, magari yenye vipaza sauti, michezo ya kuigiza na vikundi vya sanaa. Aidha, Tume kwa kutumia Mamlaka iliyopewa kisheria ya kusimamia na kuidhinisha zana za Elimu ya Mpiga Kura ambazo zinatumiwa na Asasi au Watu wanaotoa Elimu hiyo, ilipitia, kuhariri na kuidhinisha vifaa vilivyotumika katika Elimu ya Mpiga Kura. Jumla ya Asasi za kiraia 65 zilitoa Elimu ya Mpiga Kura. Kati yake Asasi za Kiraia 43 zilifadhiliwa na Shirika la Maendeleo la umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia Mradi wa Kusaidia Uchaguzi (ESP).




    1. Washirika wa Maendeleo walichangia katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kupitia Programu ya Kuimarisha Demokrasia (DDTP) na Mradi wa Kusaidia Uchaguzi (ESP). Aidha, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa ndilo lililoratibu miradi yote hiyo. Wakati huo huo Washirika wa Maendeleo wengine walitoa misaada ya moja kwa moja kwa Tume.

Kwa hiyo Tume inawashukuru sana wote waliochangia kwa hali na mali kusaidia Uchaguzi. Washirika wa Maendeleo waliochangia Programu ya DDTP walikuwa saba (7) ambao ni UNDP, DFID (UK), Sweden, Denmark, Netherlands, CIDA na Norway. Washirika wa Maendeleo waliochangia Mradi wa ESP ni Kumi na tatu (13) ambao ni UNDP, DFID(UK), Sweden, Denmark, Netherlands, Finland, Switzerland, Ireland, Canada, Belgium, European Union, Germany na Norway.




    1. Uteuzi wa Wagombea katika Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ulifanyika tarehe 19 Agosti, 2010. Kwa Uchaguzi wa Rais jumla ya Wagombea saba (7) waliteuliwa kupitia Vyama vya APPT-Maendeleo, CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na UPDP. Kwa upande wa Uchaguzi wa Wabunge na Madiwani Vyama vyote vya Siasa 18 vilishiriki katika Uchaguzi. Jumla ya Wagombea 1,036 waliteuliwa kugombea Ubunge. Jumla ya Wagombea 7,934 waliteuliwa kugombea Udiwani.




    1. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kulikuwa na jumla ya Majimbo ya Uchaguzi 239 na vituo 53,039 vya Kupigia Kura. Majimbo saba (7) hayakufanya Uchaguzi wa Bunge tarehe 31 Oktoba, 2010 kutokana na sababu mbalimbali. Uchaguzi huo ulifanyika tarehe 14 Novemba, 2010. Aidha, Uchaguzi wa Madiwani katika Kata 23 haukufanyika kutokana na ama makosa katika uchapishaji wa Karatasi za Kura au kufariki kwa baadhi ya Wagombea. Uchaguzi huo ulifanyika tarehe 28 Novemba, 2010.




    1. Tume iliandaa Maadili ya Uchaguzi ambayo, kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Maadili ya Uchaguzi yalipewa nguvu ya kisheria. Katika marekebisho hayo, maboresho yaliyofanywa ni pamoja na kuundwa kwa Kamati za Maadili katika ngazi za Kata, Jimbo, Taifa na Rufaa. Kamati hizo zilikuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa Maadili hayo.




    1. Kulikuwa na Rufaa hamsini na moja (51) zilizotokana na pingamizi dhidi ya uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi katika hatua ya Uteuzi wa Wagombea Ubunge. Kati ya Rufaa hizo jumla ya Rufaa kumi na moja (14) zilikubaliwa na thelathini na saba (37) zilikataliwa. Kwa upande wa Uchaguzi wa Madiwani kulikuwa na Rufaa 122, kati ya hizo Rufaa ishirini na mbili (22) zilikubaliwa na Rufaa 100 zilikataliwa.




    1. Kampeni za Uchaguzi zilifanyika kuanzia tarehe 20 Agosti, 2010 hadi tarehe 30 Oktoba, 2010. Kampeni ziliendeshwa kwa utulivu na kwa mujibu wa taratibu, ingawa kulijitokeza matukio machache ya fujo katika baadhi ya maeneo.




    1. Matokeo ya Uchaguzi wa Rais yalikuwa kama ifuatavyo:- Wapiga Kura walioandikishwa ni 20,137,303; Idadi Halisi ya Wapiga Kura ni 8,626,303 ambayo ni sawa na asilimia 42.84% ya Wapiga Kura wote; Kura Halali zilikuwa ni 8,398,414 ambayo ni sawa na asilimia 97.35% ya Wapiga Kura wote; Idadi ya Kura zilizoharibika ni 227,889 ambayo ni sawa na asilimia 2.65% ya Wapiga Kura wote.

Kura ambazo kila Mgombea Urais alipata kulingana na Idadi ya Kura zilizopigwa ni kama ifuatavyo:-




Mhe. Kuga, Peter Mziray wa APPT-Maendeleo

96,933

(1.12%)

Mhe. Kikwete, Jakaya Mrisho wa CCM

5,276,827

(61.17%)

Mhe Slaa, Wilbrod Peter wa CHADEMA

2,271,941

(26.34%)

Mhe. Prof. Lipumba, Ibrahim Haruna wa CUF

695,667

(8.06%)

Mhe. Rungwe, Hashim Spunda wa NCCR-Mageuzi

26,388

(0.31%)

Mhe. Mgaywa, Muttamwega Bhatt wa TLP

17,482

(0.20%)

Mhe. Dovutwa, Yahmi Nassoro Dovutwa wa UPDP

13,176

(0.15%)

Jumla

8,398,414

97.35%

Tume ilimtangaza Mhe. Kikwete, Jakaya Mrisho wa CCM kuwa amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo tarehe 5 Novemba, 2010.


Katika Matokeo ya Uchaguzi wa Rais yaliyotajwa hapo juu, asilimia iliyooneshwa ya Kura Halali ambazo kila Mgombea Urais alipata ilipatikana kwa Kutumia idadi ya Kura Halisi.
Asilimia 100% ilifikiwa kwa kujumlisha asilimia ya Kura zilizoharibika ambazo ni 227,889 (2.65%).
Ikikokotolewa kwa kutumia Kura Halali zilizotajwa hapo juu ambazo ni 8,398,414, asilimia ya Matokeo ya Uchaguzi wa Rais ambayo kila Mgombea alishinda yanakuwa kama ifuatavyo:-


Mhe. Kuga, Peter Mziray wa APPT-Maendeleo

96,933

(1.15%)

Mhe. Kikwete, Jakaya Mrisho wa CCM

5,276,827

(62.84%)

Mhe Slaa, Wilbrod Peter wa CHADEMA

2,271,941

(27.05%)

Mhe. Prof. Lipumba, Ibrahim Haruna wa CUF

695,667

(8.28%)

Mhe. Rungwe, Hashim Spunda wa NCCR-Mageuzi

26,388

(0.31%)

Mhe. Mgaywa, Muttamwega Bhatt wa TLP

17,482

(0.21%)

Mhe. Dovutwa, Yahmi Nassoro Dovutwa wa UPDP

13,176

(0.16%)

Jumla

8,398,414

100%




    1. Matokeo ya Uchaguzi wa Wabunge ni kama ifuatavyo:-

      1. CCM kilipata Majimbo 186

      2. CHADEMA kilipata Majimbo 23

      3. CUF kilipata Majimbo 24

      4. NCCR-Mageuzi kilipata Majimbo 4

      5. TLP kilipata Jimbo 1

      6. UDP kilipata Jimbo 1

Kati ya Majimbo 186 kiliyopata Chama cha Mapinduzi (CCM), majimbo kumi na saba (17) kilipita bila kupingwa.


Aidha, jumla ya Wabunge Wanawake wa Viti Maalum waliotangazwa na Tume ni 102, ambapo CCM kilipata Viti sitini na saba (67), CHADEMA Viti ishirini na tano (25) na CUF Viti kumi (10).


    1. Matokeo ya Uchaguzi wa Madiwani, Vyama vya Siasa nane (8) vilipata Madiwani kama ifuatavyo:-

      1. APPT-Maendeleo 3

      2. CCM 2,803

      3. CHADEMA 326

      4. CUF 126

      5. DP 1

      6. NCCR-Mageuzi 28

      7. TLP 20

      8. UDP 28

Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliwatangaza jumla ya Madiwani 1,184 wa Viti Maalum vya Wanawake ambao mgawanyo wao ni kama ifuatavyo:-



  1. APPT – Maendeleo 1

  2. CCM 972

  3. CHADEMA 127

  4. CUF 52

  5. NCCR-Mageuzi 11

  6. TLP 10

  7. UDP 10

  8. DP 1

Jumla 1,184


    1. Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilitoa mialiko kwa Watazamaji watarajiwa wa Uchaguzi kwa Asasi/Taasisi za nje. Jumla ya Timu za Watazamaji ishirini (20) kutoka nje walishiriki katika kutazama Uchaguzi. Shughuli za Watazamaji wa Nje ziliratibiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Pia Tume ilitoa mialiko kwa Watazamaji watarajiwa wa ndani ya nchi. Jumla ya Asasi sitini na nne (64) za ndani ambazo zilizokidhi vigezo vilivyotakiwa zilipatiwa vibali vya kutazama Uchaguzi.

Hata hivyo, ni Asasi kumi na tisa (19) tu zilizojitokeza na kupatiwa Utambulisho rasmi wa kuwa Watazamaji.




    1. Baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika hatua mbalimbali za mchakato wa Uchaguzi ni pamoja na:-

  1. Ufinyu wa Bajeti ya Uchaguzi.

  2. Ushiriki mdogo wa Wapiga kura siku ya Uchaguzi.




    1. Kwa madhumuni ya uboreshaji wa Chaguzi zijazo, Tume ina mapendekezo kadhaa miongoni mwa hayo ni:-

  1. Kuongezwa kwa Bajeti ya Uchaguzi ili ikidhi mahitaji husika.

  2. Tume kuwa na Ofisi zake katika Kanda, Mikoa na Wilaya kwa ajili ya kusogeza huduma karibu na Wapiga Kura na kuongeza ufanisi.

  3. Ugawaji wa Kata ufanyike mapema ili kuwezesha Tume kufanya Ugawaji wa Majimbo mapema.

  4. Tume inapendekeza Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ya mwaka 2010 iangaliwe upya ili kuviainisha na kuvirekebisha vifungu vinavyokinzana na Sheria za Uchaguzi.



1   2   3   4   5   6   7   8   9   ...   33


Verilənlər bazası müəlliflik hüququ ilə müdafiə olunur ©atelim.com 2016
rəhbərliyinə müraciət